TANZANIA ina vivutio vingi vya kitalii. Lakini havijatumiwa ipasavyo kuleta maendeleo tarajiwa kwa wananchi wake.
Mwaka 2003, nikiwa mwanafunzi wa Kidato cha IV katika shule ya
sekondari Kishumundu, mkoani Kilimanjaro, nilibahatika kutembelea ziwa
Chala ikiwa sehemu ya mafunzo ya somo la jiografia.
Ziwa hili lipo wilaya ya Rombo, mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Hili ni ziwa la shimoni. Ili uweze kulifikia inabidi ushuke angalau
mita 50 kutoka kilele cha vilima vilivyoko vichakani upande wa barabara
itokayo mjini Rombo.
Penya vichaka hivyo vikavu na uonyeshwe jinsi ya kulifikia ziwa.
Hapa utaanza kuona nyasi na miti na vichaka – vyote ni kijani.
Mandhari hiyo ya kijani inakusindikiza hadi kwenye ziwa.
Njia iendayo ziwani ni nyembamba; sitaki kusema ni kama ile
tunayoambiwa; ile iendayo mbinguni. Inapinda kushoto, kulia na kunyooka
mara chache sana.
Unapanda jiwe hili, jabali lile na kurudi kwenye njia nyembamba.
Inakuchukua kama muda wa dakika 25 kutoka kileleni hadi unapofika
ufukweni mwa ziwa lililozungukwa na vilima.
Hukuti watu wengi. Ni wewe na ulioshuka nao. Mwingine ni mwenye
mtumbwi mdogo na uliochakaa. Huoni shughuli zozote za uvuvi wala
kuogelea.
Lakini wakati wote ukipulizwa na upepo mwanana uvumao juu ya
maji tulivu, unafikiria jinsi ya kupanda kilima chenye mawe ili kurudi
ulikotoka.
Hapa, mwanaume mmoja wa makamo ndiye anamiliki mtumbwi pekee
ulioko ufukweni. Nakumbuka nilipotaka kazunguka kidogo ndani ya ziwa,
nilipanda mtumbwi wa mwanaume huyo – mvuvi.
Mtumbwi wenyewe ulikuwa na tundu katika kitako chake. Niliingia na kuketi. Mtumbwi ulianza kuingiza maji kupitia tunduni.
Ilimbidi mvuvi afanye kazi ya nyongeza ya kuchota na kumwaga
maji toka ndani ya mtumbwi huo kwa kopo dogo kila baada ya kupiga
makasia machache ili mtumbwi usizame.
Mandhari ya ziwa Chala yanahitaji kuendelezwa. Chala ni moja ya
maziwa yaliyotokana na mivutano ya nguvu za ardhini kama lilivyo bonde
la ufa.
Kitu kidogo kingefanyika pale. Kuweka minyororo kutoka kilimani
hadi ufukweni ikivutwa na kusukumwa na nguvu kidogo kutoka kwenye roda
(pulley) ili kuteremsha abiria chini na kuwarejesha kilimani. Hii ni
sayansi ndogo sana isiyohitaki teknolojia ya hali ya juu.
Aidha, wasimamizi wa shughuli za utalii wangeweza kuweka
mitumbwi mitatu au hata minne kufanya usafiri ziwani kuwa wa raha. Wako
wapi wapenda biashara ya utalii?
Huko ni Kilimanjaro. Kwa mara nyingine kama mwanafunzi, sasa
ikiwa mkoani Mbeya, nilipata fursa ya kufanya utafiti kwa ajili ya
kukamilisha mafunzo yangu ya Kidato cha VI. “Kwanini utalii haukui
mkoani Mbeya,” ndicho kilikuwa kichwa cha habari cha utafiti huo.
Niligundua sababu kubwa mbili. Kwanza, upungufu wa miundombinu
ya usafiri kwenda maeneo yenye vivutio hivyo vya kitalii. Pili,
kutokuwepo matangazo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo.
Ukosefu wa mambo hayo mawili umechangia watalii wengi kuishia
mikoa ya kaskazini mwa Tanzania, kwa mfano Kilimanjaro na Arusha. Huko
ndiko kuna uwanja wa ndege wa kimataifa (KIA) unaowezesha watalii kutua
karibu na vivutio.
Kuna masimulizi ya kimondo ambacho kilianguka na kinaendelea
kuwa kivutio kilichopo Mbozi mjini karibu na shule ya msingi Ndolezi.
Kuna maporomoko ya maji yaliyopo Kaporogwe wilayani Rugwe ambayo
yanaleta mandhari ya kuvutia.
Aidha, kuna “Daraja la Mungu” – kipande cha mwamba
kinachounganisha kingo za bonde na akuwa kama daraja la kisasa
lililojengwa kitaalam. Hili liko eneo la Kiwira wilayani Rungwe.
Kuna chemchemi nyingi zinazofuka maji ya moto katika eneo la
Songwe mkoani humo. Yote haya ni vivutio tosha katika mkoa wa Mbeya.
Si hivyo tu, zipo pia aina mbalimbali za mimea ya Orchids
katika hifadhi za Katavi. Moja kati ya aina ya mimea hiyo inapatikana
Tanzania peke yake; ni vivutio tosha kwa mkoa wa Mbeya.
Kuna vyura adimu wanaopatikana katika mlima Rungwe – mlima ambao
una ziwa katikati ya kilele chake. Hiki nacho ni kivutio kikubwa. Kama
vivutio hivi vyote vingekuwa vinatangazwa vizuri; na kama kungekuwa
na miundombinu ya usafiri hadi maeneo hayo, vinaweza kuchangia kwenye
pato la taifa.
Ukiacha Kilimanjaro na Mbeya, mkoa wa Mwanza, ambako pia
nimepata fursa ya kukaa, umesheheni vivutio ambavyo nimewahi
kutembelea.
Kuna kisiwa cha Saanane, kilichoko katika ziwa Viktoria. Ni
umbali wa kilometa moja kutoka bandari ya Mwanza South. Kisiwa kina
mawe yaliyopandana kiajabu na hufanya wengi kushangaa na kujiuliza kama
kweli hayakupangwa na mtu. Hapohapo Saanane kuna zuu ya wanyama
mbalimbali ambao pia ni kivutio cha kila binadamu.
Kuna vilima vya miamba na mawe yaliyopandana. Hivi vimeangaliana
na ziwa Viktoria. Ukipanda vilima hivi unaweza kuona ziwa Viktoria kwa
uwazi zaidi, kwa masafa marefu na kuburudika kwa upepo mwanana.
Fukwe za Viktoria nazo ni kivutio kwa wanaotaka kujilaza pwani
ya maji mabichi na kushuhudia jua likitua. Huu ni utajiri tosha kwa
wakazi wa Mwanza na taifa kwa ujumla.
Picha za miamba hiyo zikipigwa na kuwekwa kwenye mitandao ya
Wizara ya Utalii na Maliasili na makampuni ya utalii, zitawavuta
watalii wengi kuja kushuhudia viroja vya uasili wa Mwanza na Afrika,
kwani kuna sehemu chache duniani zenye miamba ya aina hiyo.
Lakini baadhi ya fukwe zimetelekezwa; zimejaa magugu maji kwa
kutokuwa na uangalizi mzuri. Katika maeneo mengine, hata njia kwenda
ufukweni zimezongwa na vichaka.
Miundombinu ya usafiri, hasa mitumbwi ya kupelekea watalii
katika kisiwa cha Saanane, imechakaa na chache kwa idadi. Hali hii
yaweza kumkosesha mtalii hamu ya kurudi kutembelea eneo hilo.
Kuna nchi zenye vivutio vichache duniani kama Botswana na
Mauritius lakini nchi hizo zimefaulu kuviboresha, kuvitangaza, na
kujiingizia mapato kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Tanzania
inashindwa nini?
Ili kukuza maendeleo ya sekta ya utalii, kama mchango wa sekta
hii kwa taifa, juhudi zaidi za kuboresha miundombinu katika vivutio
vya utalii sharti zipewe kipaumbele.
Muhimu ni kwa serikali na waendesha shughuli za utalii nchini,
kuandaa utalii kwa wananchi ili waweze kuona vivutio na utajiri wa nchi
yao. Utalii ni njia nyingine ya kupata elimu.
Source:Mwana Halisi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni