MWACHENI jamani. Nadhani amechoka. Mjerumani mmoja amemtetea
Mjerumani mwenzake katika kambi ya Arsenal baada ya maji kuzidi unga
pale Emirates.
Per Metersacker, beki mrefu na nguzo ya Arsenal,
amemtetea kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mesut Ozil, ambaye alikosa
penalti katika pambano dhidi ya Bayern Munich la Ligi ya Mabingwa Ulaya
huku pia akionekana kuwa katika kiwango kibovu katika maisha yake.
Arsenal ilichapwa mabao 2-0 na Bayern Munich huku
Ozil aliyenunuliwa kwa Pauni 42 milioni kutoka Real Madrid katika
kipindi cha majira ya joto kilichopita, akionekana kuwa katika kiwango
dhaifu.
Hata hivyo, Metersacker anaamini kuwa Ozil inabidi
apewe muda wa kuzoea soka la mabavu la Ligi Kuu England kwa ajili ya
kuonyesha makali yake na hana shaka kuwa ataendelea kuwa staa wa timu
hiyo.
“Tuna mechi nyingi hapa England na kila mmoja
amechoka. Lakini sio lazima Mesut tu. Ni suala la kila mtu kumtia moyo
na kumrudisha mchezoni. Wakati wa mechi tunahitaji kutiana moyo,”
alisema Metersacker.
“Mesut amecheza mechi nyingi na ni bonge la
mchezaji, tunamhitaji katika ubora wake. Mechi baada ya mechi atarudi
kuwa imara. Sio kitu cha kawaida kuja hapa na kucheza katika kiwango cha
juu katika msimu wa kwanza wenye mechi zaidi ya 50.
“Mesut ni muhimu kwetu na ni mchezaji mbunifu.
Tunahitaji pasi zake za mwisho na mabao yake, kwa hiyo kitu muhimu ni
kumtia moyo.”
Ozil alijikuta katika wakati mgumu mbele ya kiungo
Mathieu Flamini ambaye alimzonga na kumkaripia wakati wa kipindi cha
pili. Wakati huo Arsenal ilitakiwa kufanya kazi ngumu baada ya kuwa
pungufu uwanjani baada ya kipa wao kutolewa.
Mertesacker anaamini kuwa suala hilo linaonyesha jinsi kikosi cha kocha Arsene Wenger kilivyo makini uwanjani.
“Ni vizuri kutiana moyo na inabidi tufanye vizuri
kwa ajili ya timu, kuongea baina yetu ni kitu kizuri. Tunahitaji kila
mtu uwanjani awe na akili nzuri. Mathieu anajaribu kumfanya kila mtu
achangamke uwanjani. Ni vizuri kumwonyesha kila mtu kuwa uko tayari
kupigana,” alisema.
Ozil alianza vema kipindi cha maisha yake ya soka
Arsenal baada ya kuvunja rekodi ya uhamisho Emirates Septemba mwaka jana
lakini ameonekana kudorora katika siku za karibuni huku akisababisha
mabao mawili katika pambano dhidi Liverpool.
Source :Mwanaspot
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni