MKALI wa mabao wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo, Mtanzania Mbwana Samatta, amesema Mrisho Ngassa wa Yanga amefanya
kitu cha maana kwa kupiga ‘Hat-Trick’ mbili mfululizo kwenye Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Samatta alisema idadi hiyo ya mabao si kazi rahisi kwenye mashindano makubwa kama hayo.
Yanga iliifumua Komorozine ya Comoro mabao 12-2 na
kuiondosha kwenye mashindano na sasa itaikabili Al Ahly ya Misri ambayo
Samatta amesema si timu ya ajabu lakini si laini kama hakuna mipango ya
maana.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka
Lubumbashi, Samatta alisema: “Mabao sita ni mengi sana kufunga katika
Ligi ya Mabingwa Afrika, ni dalili nzuri kwake na kwa timu.
“Pia yanaashiria mambo mazuri kikubwa, lakini
asibweteke kwani anaweza kufanya kitu kikubwa katika mashindano hayo
endapo Yanga itafanikiwa kusonga mbele.
“Ngassa ni mchezaji mzuri na mwenye uzoefu, kwangu
sioni kitu cha ajabu sana kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja kwa
sababu nafahamu uwezo wake, lakini inaashiria pia kwa sasa yuko vizuri
sana kimwili na kiakili.”
Kuhusu Yanga na Al Ahly, Samatta alisema: “Al Ahly
ni timu kubwa na kama ulivyoona ni mabingwa, lakini mpira ni mchezo wa
ajabu, nina imani kama Yanga watajituma, wanaweza kuwavua ubingwa na wao
wakasonga mbele.”
Mazembe nayo imo kwenye michuano hiyo na
inajiandaa na mechi dhidi ya Astres de Douala ya Cameroon. Kuhusiana na
mchezo huo, Samatta ameweka wazi kuwa maandalizi yao ni ya nguvu.
Source: Mwanasport
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni